Unyanyasaji/Uonevu Mtandaoni (Cyberbullying)

Unyanyasaji/Uonevu Mtandaoni (Cyberbullying)

Maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasialiano (TEHAMA) yakiwemo matumizi ya Simu, Interneti, Kompyuta na Mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter na Instagram hayaepukiki duniani, na yamekuwa na faida nyingi za kijamii, kielimu, kiutamaduni, kiuchumi, na kiafya.

Tafiti zinaonesha kuwa katika nchi nyingi duniani watoto na vijana ndio watumiaji wakubwa wa vifaa vya kielektroniki na mitandao ya kijamii. Pamoja na faida ya matumizi ya vifaa vya kielektroniki na mitandao ya kijamii, matumizi yasiyo sahihi huchangia katika unyayasaji au uonevu kwenye mitandao (cyberbullying) hususan miongoni mwa watoto na vijana.

Unyayasaji au uonevu huu hufanyika pale ambapo mtu anatumia simu, Interneti au mitandao ya kijamii hutumika kwa makusudi ya kumdhalilisha au kumyanyasa mwingine. Tafiti zinaonesha kwamba watoto/vijana wengi wanatabia ya kuwanyanyasa wenzao kwenye mitandao kwa kuweka au kutuma picha au video za kudhalilisha, kusambaza taarifa za uzushi/umbea na uongo, kutumia lugha na jumbe za matusi, kejeli na dhihaka ikiwemo kutoa maoni ya kuudhi kwa lengo la kumchafua au kumfanya mtu mwingine ajisikie vibaya. 

Tafiti za awali kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza nchini Tanzania zinaonesha kuwa watoto wa 4 kati ya 10 wanaotumia simu na Interneti wamejihusisha na vitendo vya kuwanyayasa wengine mtandaoni na watoto 6 kati ya 10 wamekiri kupitia manyayaso au ukatili mtandaoni (Onditi, 2017; Onditi, 2018; Onditi & Shapka, 2019). Uonevu au ukatili mtandaoni umekua na athari hasi kwa watoto ikiwemo wasiwasi/hofu, maendeleo yasiyoridhisha shuleni, mahusiano mabaya, kutokujiamini, upweke, msongo wa mawazo, sonona, fikra za kujiua, na hata hupelekea kujiua. Hivyo, matumizi ya vifaa vya kielektroniki na mitandao ya kijamii imewaweka watoto mahala ambapo si salama kwa ustawi na makuzi bora iwapo itaendelea kutumika visivyo.

 

UJUMBE

Watoto

Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa mtoto hayakwepeki, hivyo unawajibika kutumia teknolojia hii lakini kwa kuzingatia matumizi sahihi kwa mujibu wa taratibu na miongozo mliyowekewa. Matumizi mabaya yanaweza kuumiza wengine mfano lugha za kejeli, kudhalilisha na kusambaza taarifa za uongo dhidi ya mwenzio. Epuka kutuma au kusambaza picha, video au taarifa za mtu mwingine bila ridhaa yake; hii ni kinyume cha sheria za mitandao na haki ya mmiliki halisi wa taarifa hizo. Pia, epuka kutuma taarifa zako muhimu au binafsi, mfano anuani ya makazi, namba ya simu, ratiba za wazazi, barua pepe na nywila; hakikisha hautumi picha zako au za wengine za utupu au kujirekodi mubashara mtandaoni kwa lengo la kumuonyesha mwingine mtandaoni, hata kama ni rafiki wa karibu sana. Kufanya hivi kunaweza kukuingiza katika mikono ya wahalifu mitandaoni; kumbuka chochote unachokituma kwenye mitandao hakifutiki, kitaondoka tu kwenye chombo unachotumia na hivyo kukuweka katika hatari kwa taswira yako kutumika wakati wowote katika maisha yako. Aidha, epuka kutumia muda mwingi kwenye Interneti na mitandaoni kwa kujiburudisha, kucheza gemu, au kuwasiliana na wengine hii itakuepusha na matatizo ya kiafya na urahibu (addiction). Aidha, epuka tabia ya kupakua program tumishi (Applications) ambazo hujui chanzo chake bila kumshirikisha Mzazi/mlezi, mwalimu au mtu mwingine mwenye ufahamu na masuala haya lakini pia unayemwamini.

 

Epuka kuwa na marafiki usiowafahamu mtandaoni kwani wanaweza wakakurubuni, pia usikubali ombi la kukutana na mtu uliyekuwa unawasiliana naye ana kwa ana nje ya mitandao kwani anaweza kuwa hatari kwa usalama wako. Tafadhali toa taarifa kwa wazazi/walezi, mwalimu, Jeshi la Polisi-Dawati la Jinsia na watoto au piga simu ya bure namba 116 kwa msaada wa haraka iwapo mtu usiyemfahamu anataka ufanye mambo yasiyo ya kimaadili ikiwemo kutuma picha zako mtandaoni. Upatapo habari au taarifa usiyokuwa na uhakika nayo mtandaoni hakikisha hauizambazi sehemu nyingine, na kama taarifa hiyo ina ujumbe wa utata basi tuma message picha (emoji) pamoja na ujumbe huo. Ukiwa kwenye mitandao ya kijamii zingatia usiri wa akaunti yako na taarifa zako kwa kutumia “private settings.” Kadhalika, hifadhi kumbukumbu za mawasiliano ya picha, ujumbe, video za kuudhi/kudhalilisha mtandaoni kwa ajili ya ushahidi na msaada zaidi utakapohitajika. Zingatia kuwa, kabla ya kubonyeza kitufe cha tuma ujumbe fikiri kwanza namna ambavyo utajisikia endapo wazazi wako, ndugu zako, rafiki zako wataziona taarifa ulizosambaza kwenye mitandao.

 

WAZAZI/WALEZI

Mzazi/Mlezi hakikisha una uelewa wa kutosha kuhusu kifaa cha kielektroniki na majukwaa yaliyopo mtandaoni ambayo mtoto anatumia ili kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mtandao na kutoa msaada pale unapoona mtoto anahitaji msaada wako. Aidha, Mzazi/Mlezi hakikisha unatengeneza muongozo wa kifamilia kuhusu matumizi sahihi na salama ya vifaa vya kielektroniki ikiwemo simu, kompyuta, tablet na namna bora ya kutoa taarifa pale ambapo kuna taarifa zisizo za kawaida. Vile vile, ni muhimu kuwafundisha watoto namna bora ya mawasiliano na kutokutumia lugha za matusi, kibaguzi, maudhui ya kingono mtandaoni kwa kuwa ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya kimtandao namba 14 ya mwaka 2015. Mzazi/Mlezi unapaswa kuwa na mawasiliano ya karibu na mtoto wako, mlinde, na zungumza naye ili kujua yanayomsibu kabla tatizo halijawa kubwa. Toa taarifa kwa Jeshi la Polisi-Dawati la Jinsia na watoto au piga simu ya bure namba 116, eleza tatizo lako ili kupata msaada wa haraka. Mzazi/Mlezi epuka kutuma picha za mtoto wako akiwa katika hali yeyote ile mfano mtoto akiwa uchi, mchafu au akifanyiwa ukatili kwani inamdhalilisha, kwa kuwa wahalifu wa mtandao wanaweza kuitumia wakati wowote katika maisha ya mtoto. Picha ya mtoto itabaki katika mtandao katika maisha yake yote japokuwa unaweza kuiondoa katika chombo unachotumia. Mzazi/Mlezi hakikisha unasimamia muda wa mtoto kutumia simu, mitandao, vifaa vya kielektroniki ili kumuepusha na usugu wa kutamani kuendelea kutumia, yaani urahibu.

 

Welcome to official site of Safer Internet Tanzania, a home of safer internet day, hosted and managed by Computing and Information Association.

 

Wasiliana Nasi

  •  Plot No 2AE 20, Nyerere Road, Opposite Quality Motors.
  • Phone 1 0756 348  364
    Phone 2 : 0758 707 370