Ukatili Wa Watoto Kingono Mitandaoni (Online Child Sexual Exploitation And Abuse)

Ukatili Wa Watoto Kingono Mitandaoni (Online Child Sexual Exploitation And Abuse)

Maendeleo na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano nchini na duniani kwa ujumla, imesababisha kuwepo kwa matumizi yaliyo sahihi na yasiyo sahihi ya mitandao na vifaa vya kielektroniki. Kutokana na uelewa mdogo kuhusu matumizi sahihi na salama ya mitandao na vifaa vya kielektroniki, tunashuhudia usambazwaji wa picha mnato, video za ngono, maandishi ya kingono, muziki na kazi nyingine za sanaa zenye maudhui ya kingono.

Ni hatari kwa mtoto akiona maudhui hayo kwa kuwa anaweza kuiga na kuanza kujaribu; hatimaye hujikuta akishiriki ngono katika umri mdogo. Aidha, kuna baadhi ya watu katika jamii humshawishi mtoto ili kumpiga pichaau kumrekodi au kujipiga picha/kujirekodi zenye mwelekeo wa kingono na kuzisambaza mitandaoni; picha hizo zina athari kwa mtoto anapoziona ikiwa ni pamoja na kuchochea mihemko kwa watoto na kuanza kushiriki ngono katika umri mdogo; pia inaweza kushawishi mtoto kujifunza ushiriki wa ngono ya jinsi moja na hata kinyume na maumbile ikiwa picha/filamu hizo zina mwelekeo huo, mtoto anapoona huamini kwamba, vitendo hivyo ni vya kawaida na hivyo kuendelea navyo. Aidha, imesababisha mmomonyoko mkubwa maadili ya kitanzania kwa watoto ambao kunasababishwa na kuiga mambo mbalimbali yasiyofaa mitandaoni. Katika matumizi ya muda mrefu mitandaoni, watoto wamejikuta na urahibu wa mitandao ambao umepunguza muda wa kujisomea na hatimaye kushusha kiwango cha ufaulu.

 

Kadhalika, kuna baadhi ya watu humshawishi mtoto kupiga au kujipiga picha/filamu zenye mwelekeo wa kingono na kuzimiliki. Picha/filamu hizo zinaweza kutumika kumtisha mtoto ili asitoe taarifa kwa wazazi/walezi au mtu yeyote anaye mwamini; na iwapo atafanya hivyo mhusikia anaweza kuzisambaza; lengo likiwa kushiriki naye ngono au kupata fedha. Kutokana na hali hiyo, mtoto huendelea kurubuniwa na kufanyiwa ukatili bila kutoa taarifa au kuomba msaada; hali hii isipodhibitiwa, husababisha msongo wa mawazo kwa mtoto unaoweza kusababisha kujiua.

 

Yakuzingatia

Mtoto

Mtoto unapaswa kutambua kwamba matumizi ya vifaa vya kielektroniki yana faida katika kujifunza na kukuongezea ujuzi. Kumbuka, kutoa taarifa zozote zinazokuhusu mtandaoni ni hatari kwa usalama wako. Aidha, epuka kutumia muda mrefu mtandaoni ili kujizuia na urahibu utakaokupotezea muda wa kujisomea na kuwasaidia wazazi. Urafiki na mtu yeyote usiyemfahamu mtandaoni ni hatari kwa usalama wako, muepuke. Ukihisi usalama wako upo hatarini katika mitandao, piga simu namba 116 ili kupata msaada, pia toa taarifa kwa mzazi/mlezi, mwalimu, mtu unayemwamini, kiongozi (kama afisa ustawi wa jamii, wajumbe na wenyeviti wa serikali za mitaa) aliye karibu na wewe au kituo cha polisi – dawati la jinsia na watoto. Hakikisha, hautumi au kuhifadhi picha au video zenye maudhui ya kingono, hilo ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria Na 14 Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

 

Mzazi/Mlezi

Mzazi/mlezi epuka kutoa taarifa zozote za mtoto wako mtandaoni ni hatari kwa usalama wa mtoto na pia kila wakati zungumza na mtoto kuhusu matumizi sahihi ya mtandao. Aidha, Mzazi/mlezi hakikisha kuwa mtoto anatumia simu na vifaa vya mawasiliano chini ya uangalizi wako na ikibidi vifaa hivyo viwekwe nywila. Vile vile, tambua kuwa kumrekodi mtoto, kutunza au kutuma picha zenye maudhui ya ngono ni kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya Mwaka 2015 Kifungu cha 13(1) ambapo adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni hamsini au kifungo kisichopungua miaka saba (7) au vyote viwili kwa pamoja. Pia ni kinyume na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 kifungu cha 33 na adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni mbili na isiyozidi milioni kumi na tano au kifungo cha miaka mitatu au vyote viwili kwa pamoja.

Wadau na Jamii

 

Wizara ya Elimu ina wajibu wa kufanya mapitio ya mitaala ili kujiridhisha kama inakidhi mahitaji ya sasa kwa kutoa fursa kwa mtoto kujifunza elimu ya matumizi sahihi ya mtandao (digital literacy) ikizingatia matumizi ya vifaa vya kielekroniki na mitandao kwa lengo la kuendana na kasi ya maendeleo ya kidijitali duniani. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na vyombo vingine vya utekelezaji kama polisi na mahakama vihakikishe kwamba sheria zinasimamiwa vema katika kukabiliana na uchapishaji, utumaji na usambazaji wa maudhui ya kingono dhidi ya watoto. Aidha, Mamlaka zinazohusika zina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na miongozo kuhusu matumizi ya mitandao ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa Watoto. Aidha, kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo ili kukidhi haja ya kasi ya mabadiliko yanayotokea.

 

Mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla mna nafasi na jukumu kubwa la kumlinda mtoto dhidi ya athari za mitandao na vifaa vya kielektroniki kwa kuwaelimisha wazazi/walezi namna matumizi yasiyo sahihi ya TEKNOHAMA yanavyoweza kuathiri malezi, makuzi na maendeleo ya Watoto katika jamii. Aidha, Jamii inajulishwa uwepo wa simu ya bure namba 116 kwa ajili ya kuripoti usambazwaji wa picha au tukio lolote lenye madhara kwa mtoto mtandaoni au toa taarifa kituo cha polisi dawati la jinsia na watoto, pia unaweza kutoa taarifa ofisi za serikali za mitaa.

Jamii inapaswa kutambua kwamba Sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 inalinda haki zote za mtoto kama zilivyoainishwa katika Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008. Aidha, jamii inafahamishwa kuwa Sheria Na 14 ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha 13(1) kinakataza kuweka au kuwahusisha watoto na maudhui ya Kingono. Vile vile, Shule zihakikishe zinatekeleza miongozo kuhusu matumizi ya vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Kadhalika, jamii inaaswa kuzingatia maadili na malezi ya kitanzania, bila kuathiriwa na utandawazi. Ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha kwamba inashiriki kwenye masuala yanayohusu usalama wa watoto katika mitandao.

Jamii inapaswa kutambua na kutumia njia za kutoa taarifa za ukatili wa kingono wa mtandao ikiwemo simu ya bure ya serikali 116 na kutumia wavuti ya Internet Watch Foundation – IWF ili kuripoti maudhui ya kingono mtandaoni ili yaweze kuondolewa.

 

Welcome to official site of Safer Internet Tanzania, a home of safer internet day, hosted and managed by Computing and Information Association.

 

Wasiliana Nasi

  •  Plot No 2AE 20, Nyerere Road, Opposite Quality Motors.
  • Phone 1 0756 348  364
    Phone 2 : 0758 707 370