Matumizi Ya Luninga Kwa Mtoto (TV Usage For Child)

Matumizi Ya Luninga Kwa Mtoto (TV Usage For Child)

Luninga ni chombo chenye historia kubwa katika tasnia ya habari na mawasiliano Duniani. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa sasa kuna Luninga zenye uwezo wa kutumia internet sawa na kompyuta au simu-runinga janja (Smart TV). Kutokana na juhudi za Serikali katika kusambaza umeme hadi vijijini, kuna uwezekano mkubwa wa familia nyingi za kitanzania kumiliki chombo hiki kama ilivyo kwa simu za mkononi (smart phones). Uwepo wa nishati ya umeme, umesababisha kuongezeka kwa vibanda vya kuonesha sinema, maarufu kama vibanda umiza katika maeneo mbalimbali mijini na vijijini ambavyo watumiaji wake wakubwa ni watoto. Ni dhahiri kuwa matumizi mahsusi ya luninga kwa Jamii yetu wakiwemo watoto ni kwa ajili ya kupata habari, maarifa na burudani. Lakini, kuna udhibiti mdogo sana wa maudhui yanayooneshwa katika vibanda hivyo “ukiona tangazo lina neno kuna kachumbari, picha za ngono zinaoneshwa hapo”

Vilevile, vyombo vingi vya usafiri hasa mabasi ya abiria yamekuwa yakionesha sinema kwa kutumia luninga. Lakini baadhi ya sinema hizo hazizingatii maudhui sahihi kwa watazamaji wakiwemo watoto. Pamoja na faida za luninga, kumekuwa na athari hasi hususani kwa watoto hasa pasipokuwa na uangalizi au mwongozo wa kutumia chombo hiki, ambapo huwaweka watoto kwenye hali hatarishi kimakuzi na kimaadili.

Bila kuchukua hatua stahiki na za haraka kwa kudhibiti Maudhui yasiyofaa katika luninga majumbani, vyombo vya usafiri na kwenye vibanda vya sinema; husabisha watoto kujifunza au kuiga matendo na tabia zisizofaa na kukubalika kwenye Jamii yetu. Tabia hizo ni pamoja na ubakaji, ulawiti, ugomvi, chuki, lugha chafu, mavazi yasiyo na staha na kuangalia picha za ngono zinazopelekea hisia za ngono kwa watoto. Hali hii inaweza kutufanya kuwa na jamii/ kizazi kisichokuwa na maadili na chenye ongezeko la uhalifu na ukatili katika jamii.

YAKUZINGATIA

Mtoto

Mtoto omba ruhusa au mtaarifu mzazi/mlezi kabla ya kwenda kutazama vipindi/filamu ili mzazi au mlezi aweze kujiridhisha na maudhui yaliyomo katika kipindi/filamu unayokwenda kuangalia. Aidha, mtoto mueleze au toa taarifa kwa Mzazi /Mlezi juu ya tabia na matendo yasiyofaa au yanayokupa mashaka unayoyaona kwenye luninga ili Mzazi au Mlezi achukue hatua. Vile vile, zingatia ratiba ya kutazama luninga, ili upate muda wa kujisomea, kucheza na kusaidia Wazazi/walezi kazi za nyumbani.

 

 

 

Mzazi/Mlezi

Mzazi /mlezi panga ratiba ya mtoto kuangalia luninga ili kumpa nafasi mtoto kufanya mambo mengine, lakini pia kumwepusha na uwezekano wa kukumbwa na urahibu na hata ongezeko la uzito kwa kukaa muda mrefu kuangalia luninga. Aidha, Mzazi/Mlezi fuatilia maudhui ya vipindi vya moja kwa moja (Mubashara/Tamthilia) vinavyotazamwa na mtoto kwenye luninga ili kutoa ushauri unaofaa kulingana na umri wake. Vile vile, jiwekee utaratibu wakupitia vipindi au nakala za video /CD kabla ya kuruhusu mtoto kutazama ili kujua maudhui kama ni sahihi kwa Mtoto. Kadhalika, epuka kuweka nakala za video /CD zenye maudhui ya kiutu uzima mahali ambapo mtoto anaweza kuzifikia kirahisi na kuzitamaza  bila wewe kujua. Jenga tabia ya kutazama luninga pamoja na Mtoto wako kwenye vipindi vyenye maudhui ya kujenga na muelimishe pale mbapo kitendo kiovu/kibaya kimeonekana kwenye luninga. Mzazi/Mlezi una jukumu la kujua ni wapi na ni sinema inayoonyeshwa kwenye  VIBANDAUMIZA ina maudhui gani  kabla ya kumruhusu Mtoto. Na iwe muda wa mchana pekee kwa ratiba mtakayokubaliana.

 

Mamlaka za Serikali

Mamlaka zinazohusika na udhibiti wa maudhui mitandaoni zikiwemo Bodi ya filamu, BASATA, TCRA na LATRA kuendelea kuhakiki maudhui ya vipindi au CD zinazolenga watoto ili kuepusha upotoshaji wa maadili. Wizara ya Elimu iendelee kuboresha miongozo ya matumizi ya vifaa vya kieletroniki shuleni ikiwemo matumizi ya luninga kwa kuzingatia maudhui ya vipindi vinavyooneshwa. Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuangalia utimilifu wa mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji wa majumba ya sinema ili kudhibiti uanzishwaji holela ambao udhibiti wake unakuwa hafifu. Aidha, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na LATRA kutengeneza utaratibu wa kufuatilia maudhui ya video zinazooneshwa kwenye vyombo vya usafiri. Vile vile, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia TCRA kuona uwezekano na utaratibu wa watoto kudhaminiwa na wazazi wao kumiliki namba za simu. Kadhalika, Serikali za Mitaa zitunge Sheria ndogo zitakazosimamia na kudhibiti uanzishwaji na uendeshaji wa Vibanda vya Sinema bila kumuathiri Mtoto. Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Wadau waanzishe Vituo vya Burudani vya Watoto ili kuwapa fursa ya kucheza na kuwapunguzia Urahibu wa kutazama Runinga.

Watoa Huduma

Watoa huduma ya kurusha Matangazo (Visimbuzi/Ving’amuzi) kuhaikisha miongozo inakuwepo ya vipindi vinavyomlenga na visivyomlenga Mtoto. Mfano, waweke wazi ni mtoto wa umri gani anapaswa kuangalia na kuna maudhui gani kwenye kipindi husika.

Aidha, Wazingatie muda na wakati muafaka kwa kuonesha vipindi visivyomlenga mtoto ili kumuepusha kutazama maudhui yasiyomfaa. Kwa mfano vipindi au filamu zenye maudhui yenye mwonekano wa kumwathiri mtoto ni vyema vikaonyeshwa wakati mtoto amelala. Hili likijulikana kwa kila mzazi/mlezi atahakikisha mtoto hahusiki katika vipindi au filamu hizo. Watoa huduma  wote wanapaswa kuwa na dawati la huduma kwa wateja/walaji kwa ajili ya kupokea na kushughulikia malalamiko yao juu ya maudhui na huduma yao. Aidha, wamiliki wa vibanda vya sinema wazingatie sheria na haki za Mtoto kwa kutoonesha maudhui yasiyofaa na kutowaruhusu kuingia kwenye vibanda hivyo muda wa usiku.

 

 

Welcome to official site of Safer Internet Tanzania, a home of safer internet day, hosted and managed by Computing and Information Association.

 

Wasiliana Nasi

  •  Plot No 2AE 20, Nyerere Road, Opposite Quality Motors.
  • Phone 1 0756 348  364
    Phone 2 : 0758 707 370