Kurubuni Watoto Mtandaoni (Online Grooming)

Kurubuni Watoto Mtandaoni (Online Grooming)

Tanzania ni mojawapo ya nchi inayotumia vifaa vya kielekroniki na mitandao kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa mwaka 2018, jumla ya Watanzania wapatao 23,142,960 sawa na 43% walijiunga na mitandao. Aidha, idadi kubwa ya watumiaji hao hawana uelewa wa kutosha kuhusu matumizi salama ya mitandao. Watoto ni miongoni mwa kundi hilo, ambao hujikuta wanatumia mitandao hiyo kuanzisha urafiki na watu wasiowafahamu.

Katika urafiki huo, watoto wengi wamerubuniwa nakujiingiza katika mahusiano ya kingono mitandaoni. Kumekuwepo na udhibiti mdogo wa mitandao ambayo inachangia kuhatarisha usalama wa mtoto katika mitandao. Mfano, picha na taarifa binafsi za watoto huweza kutumwa katika mitandao ambazo huweza kutumika kuwarubuni watoto ili kushiriki ngono mitandaoni. Aidha, mtoto anaweza kurubuniwa na kujikuta wakionana na wahalifu wa kingono ana kwa ana na hivyo kumfanyia ukatili.

Athari kubwa ya kurubuniwa mitandoni, ni pamoja na kuanza kufanya ngono katika umri mdogo na hata kuanza biashara ya ngono, athari nyingine ni kujiingiza katika usafirishaji haramu wa watoto, matumizi ya madawa ya kulevya, msongo wa mawazo unaoweza kusababisha mtoto kujiua. Kwa kuwa, Wazazi/walezi na walimu waliowengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu matumizi sahihi ya mtandao, hivyo hawafuatilii jinsi watoto wanavyotumia vifaa vya kielektroniki na mambo wanayoyafanya kwenye mitandao. Kutokana na hofu na kuamini kwamba wazazi, walezi au walimu hawana ufahamu wa kutosha, watoto hawawashirikishi mambo wanayoyafanya au wanayokutana nayo mitandaoni. Tumeshuhudia watoto kurubuniwa mitandaoni; na hatua za haraka zisipochukuliwa, tutashuhudia madhara makubwa kwa watoto wetu. 

Yakuzingatia

Mtoto

Mtoto akiwa sehemu ya jamii anawajibika kutumia vifaa vya kielektroniki na mitandao ili kupata taarifa zenye manufaa kwake hasa masomo, hivyo basi ni jukumu la Wazazi/walezi, walimu na jamii kwa ujumla kuhakikisha mtoto anatumia mitandao kwa usahihi. Mtoto hakikisha, ni taarifa sahihi tu unazopokea na kuzisambaza; kwa kuwa taarifa zisizo sahihi unazoziweka kwenye mitandao zitaendelea kuwepo katika mitandao hiyo maisha yako yote hata ukizifuta kwenye kifaa unachotumia, zitaendelea kubaki.

Aidha, unashauriwa kutowasiliana wala kukutana ana kwa ana na mtu yeyote usiyemfahamu, ikiwa utalazimika kukutana naye sindikizwa na mtu unayemwamini ambaye anaweza kuwa mzazi/mlezi au mwalimu. Vile vile, unaweza kuchukua hatua ya kumfungia (kum-block) mtu yeyote ambaye unaona anakusumbua kwa maneno, picha au tabia isiofaa mtandaoni.

Wazazi/Walezi

Mzazi/Mlezi mnapaswa kufahamu matumizi sahihi ya vifaa vya kielektroniki na mitandao inayotumiwa na mtoto/watoto wako ili kutoa ushauri, maelekezo na kusimamia matumizi sahihi. Aidha, weka kompyuta au kifaa cha kielektroniki chenye mtandao kwenye sehemu ya wazi kama sebule na kuhakikisha mtandao unapatikana sehemu ambayo utakuwa na uangalizi nayo. Vile vile, ongea na watoto kuhusu jinsi ya kujilinda wakiwa mitandaoni na athari ambazo wanaweza kuzipata kutokana na kutuma picha au taarifa zao mitandaoni, kukutana au kuchati na watu wasiowajua mitandaoni. Kadhalika, mzazi/mlezi kubaliana na mtoto ili kuweka utaratibu wa masaa ambayo watoto wanapaswa kuitembelea mitandao. Kutokana na umri wa mtoto, aelekezwe kutumia mitandao maalumu ya Watoto kama vile YouTube-kids, Kiddle na safe-search kids na mingineyo. Mzazi/Mlezi unashauriwa kujenga urafiki wa karibu na mtoto ili aweze kukushirikisha vitu/masuala  anayokumbana nayo kwenye mtandao.

Walimu:

Walimu mnapaswa kuweka kompyuta au vifaa vya kielektroniki vyenye mtandao kwenye sehemu ya wazi kama darasani, na hakikisha mtandao unapatikana sehemu yenye uangalizi ili kuwalinda watoto kutojiingiza katika matumizi yasiyo sahihi ya mitandao. Aidha, walimu mnapaswa kufahamu mitandao ambayo wanafunzi wanaitembelea na muda wanaotumia kuwa mitandaoni. Walimu ongeeni na wanafunzi kuhusu namna ya kujilinda wakiwa mitandaoni na athari ambazo wanaweza kuzipata kutokana na kutuma picha au taarifa zao na kukutana au kuchati na watu wasiowajua mitandaoni. Walimu hakikisheni kunakuwepo na mijadala inayohusu faida na hasara za matumizi ya mitandao na hakikisha wanafunzi wanafuata miongozo ya Elimu kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kielektroniki. Shule zinapaswa kuwa na ‘web content filters’ kwenye mtandao wa shule ili wanafunzi wasitumie mitandao isiyofaa.

Mamlaka ya Mawasiliano:

TCRA, mshauriwa kuongeza juhudi katika kusimamia na kuchukua hatua za kisheria kwa mitandao ambayo ina maudhui ya kingono na maudhui mengine yasiyoendana na utamaduni wa kitanzania ili kuwalinda na kuwaweka watoto salama mitandaoni ikiwa pamoja na kurubuniwa kwa watoto kingono mitandaoni.

 

Welcome to official site of Safer Internet Tanzania, a home of safer internet day, hosted and managed by Computing and Information Association.

 

Wasiliana Nasi

  •  Plot No 2AE 20, Nyerere Road, Opposite Quality Motors.
  • Phone 1 0756 348  364
    Phone 2 : 0758 707 370